JESHI la Wananchi Tanzania (JWTZ), limesema limeanza kuwapeleka askari wake nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) kulinda amani na kuhakikisha wananyang’anywa silaha zote waasi wa kundi la M23 ili nchi hiyo itawalike.
Kutokana na hatua hiyo, JWTZ limesema halitishwi na vitisho vya M23 kutokana na kujiandaa vizuri kila idara, ikiwa ni lengo la kutaka kuona wananchi wa DRC wanaishi kwa amani, tofauti na sasa ambako kumekuwa na vitendo vya kinyama dhidi ya wanawake na watoto wadogo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, wakati wa kutoa tamko la jeshi hilo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema kamwe hawatishwi na kundi la M23.
Alisema wanashangazwa na kitendo M23 kutoa vitisho, wakati askari wanaokwenda huko wanatoka nchi za Afrika Kusini, Malawi na Tanzania.
“Kwa nini iwe Tanzania pekee, sisi hatuwezi kutishwa na kikundi cha wanamgambo 1,000, tunasema tunakwenda kutimiza jukumu la Umoja wa Mataifa (UN) kuhakikisha DRC inatawalika na silaha zote wananyang’anywa,
“Tanzania tuna historia kubwa ya kuleta ukombozi na amani ndani ya nchi za Afrika, zikiwamo Commoro, Afrika Kusini, Liberia, Sudan na Lebanon, ndiyo maana vikosi vyote vitatu vinaongozwa na Mtanzania, Brigedia Jenerali James Mwakibolwa.
“Tulipokwenda Commoro, tulihisi kama damu itamwagika lakini hali ilikuwa tofauti kabisa na isitoshe ni askari mmoja tu aliteleza na kuanguka majini, sasa hawa M23 wao wamepata wapi mafunzo.
“Itakumbukwa Idd Amin Dada, alikuwa anajigamba na kusema anataka kuja kunywa chai Dar es Salaam, lakini aliishia kuchungulia visiwa vya Ukerewe… majigambo ya M23 ni ishara ya kuanza kuwa na wasiwasi,” alisema Kanali Mgawe.
Alisema kikosi kilichoanza kwenda DRC,kinajulikana kama Tanzania Bataria One –DRC (TANZBATT-1 DRC) na kuongeza kwamba kila baada ya miezi sita kutafanyika mabadiliko kadri itakavyohitajika.
Alisema kutokana na vitisho hivyo, bado Tanzania ni salama na itakuwa kuwa salama na kuwataka Watanzania kuondoa hofu juu ya matukio yanayotokea hivi sasa.
Alisema vifaa vya askari, wanaokwenda Kongo vimekamilika na tayari UN imevifanyia ukaguzi na kuridhia vinakidhi mahitaji katika kuimarisha ulinzi na usalama.
Kuhusu mzozo wa Tanzania na Malawi, alisema nchi hizo bado zina uhusiano mzuri wa kidiplomasia.
Mapema wiki hii, Rais Jakaya Kikwete aliwakabidhi askari wa JWTZ bendera mkoani Pwani, ikiwa ni ishara ya kuanza safari ya kuelekea DRC.
No comments:
Post a Comment