Nairobi. Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya nchini Kenya imeagiza kuchunguzwa kwa fomu 34 za matokeo ya uchaguzi wa rais kutoka katika vituo vyote 34,400, vilivyotumika kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Machi 4, mwaka huu.
Kadhalika mahakama hiyo jana iliagiza kuhesabiwa upya kwa kura za urais katika vituo vya kupigia kura 22 kati ya elfu 33 vilivyolalamikiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Muungano wa Cord, Raila Odinga.
Katika malalamiko yake yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo kupinga Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Machi 4, Odinga alidai kuwa vituo hivyo 22 kura zilizopigwa zinazidi idadi ya wapigakura walioandikishwa.
Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya majaji wenzake watano, Jaji Smokin Wanjala alisema kwamba uhesabuji kura wa vituo hivyo utafanyika leo kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu madai hayo.
“Matokeo ya kura zitakazohesabiwa katika vituo hivyo 22 yawasilishwe katika mahakama hii Jumatano, saa 10.00 jioni,” alisema Jaji Wanjala.
Kikao hicho, ambacho Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande amealikwa kama mwangalizi, ni cha awali kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa rasmi keshokutwa (Alhamisi) na kuendelea kwa mfululizo hadi kufikia uamuzi ikiwa madhumuni yake.
Lengo ni kupitia madai yaliyowasilishwa mahakamani hapo na pande zote zinazohusika na kuamua mwenendo wa kesi utakavyofanyika.
Ukiachilia mbali kesi iliyofunguliwa na Odinga kupinga Kenyatta kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa tano tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa Kenya, kuna kesi nyingine ambayo imefunguliwa na muungano wa mashirika yasio ya kiserikali, `The African Centre for Open Governance’ (Africog).
Katika kesi hiyo inayorushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni nchini Kenya, Africog inahoji uhalali wa uchaguzi huo.
“Kesi yetu haihusiani na nani ameshinda au kushindwa bali jinsi umma ulivyoshindwa, tumepoteza ahadi ya uchaguzi uliowazi,” alisema Gladwell Otieno, Mkurugenzi Mtendaji wa Africog.
Kesi ya tatu ambayo imefunguliwa na wajumbe wa timu ya kampeni ya Kenyatta, mwanaharakati katika mitandao ya kijamii Dennis Itumbi na Moses Kuria wanaopinga uamuzi wa Tume Huru ya uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya kujumuisha kura zilizoharibika wakati wa kujumlisha kura za wagombea urais.
Katika uamuzi wake, mahakama iliamua kwamba kesi zote tatu zitaunganishwa kuwa moja, huku ile iliyowasilishwa na Odinga ikiwa ndiyo kinara wa kesi zote.
Pia mahakama iliamuru Muungano wa Vyama vya Siasa wa Cord na Jubilee kuteua mawakala 10 kila mmoja ambao watakula kiapo mahakamani hapo kabla ya kuanza kuhesabu upya kura hizo.
Katika uamuzi wake jana jioni, mahakama hiyo ilikubali ombi la Mwanasheria Mkuu wa Kenya, kushiriki katika kesi hiyo kama rafiki wa mahakama na siyo mdaiwa kama ilivyokuwa awali. Wakili wa Cord, George Oraro alikubali uamuzi huo licha ya kuupinga awali.