Thursday, April 25, 2013

FFU WAACHA LINDO NA KUINGIA DISCO KUKATA MAUNO



ASKARI Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Kilimanjaro wanaolinda mipaka kukabiliana na biashara za magendo zisiende Kenya, wanadaiwa kuacha lindo na kutinga ukumbi wa disko wakiwa na silaha nzito za kivita aina ya SMG.
  
Tukio hilo lilitokea usiku wa Aprili 20 mwaka huu, ambapo askari hao zaidi ya watano waliingia katika ukumbi wa disko wa High Way uliopo njia panda ya Himo na hivyo kutoa mwanya kwa magari sita aina ya Fuso yaliyokuwa yamesheheni sukari ya magendo kupita kirahisi kwenda nchini Kenya.
  
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa baada ya askari hao kutinga katika ukumbi huo, ilichukua muda wa dakika 20 magari yakaanza kupita eneo hilo ambako askari hao walikuwa wameweka doria katika barabara ya Mwika.
  
Mbali na askari hao, pia maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nao huweka doria katika barabara hiyo ya Mwika, lakini siku hiyo waliungana na askari wale katika ukumbi wa disko na kuacha magari hayo yakienda Kenya bila kukaguliwa.
  
Hata hivyo, raia wema waliwasiliana na waandishi wa habari za uchunguzi ambapo magari mawili yalijikuta mikononi mwa wananchi huku moja likiwaponyoka baada ya dereva wake kukimbia na kwenda kulificha katika mji mdogo wa Himo.
  
Gari lililobaki mikononi mwa wananchi wakiwamo pia waandishi wa habari za uchunguzi lilikuwa na namba za usajili T 695 BXH aina ya Fuso mali ya Susan Bahati Paul wa Moshi Mjini ambalo lilibainika kusheheni sukari kutoka nchini Thailand.
  
Gari hilo ambalo lilikuwa mita chache kuingia nchini Kenya kupitia eneo la machimbo ya mchanga aina ya pozolana, lilikabidhiwa kwa maofisa wa TRA katika kituo cha forodha cha Holili likiwa na mifuko 250 ya sukari yenye ujazo wa kilo 50 kia moja.
  
 Alipoulizwa jana juu ya askari wake kwenda kustarehe disko na kuacha sukari ikienda Kenya, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita pamoja na kudai hana taarifa, aliahidi kulishughulikia suala hilo.
  
Wakati Moita akidai hana taarifa, habari za ndani ya Jeshi la Polisi zimedokeza kuwa askari wote waliokuwa zamu mpakani hapo usiku wa kuamkia Aprili 20 mwaka huu, wamehojiwa juu ya tuhuma za kuachia magari hayo yaliyosheheni sukari ya magendo.
  
Taarifa hizo zimedokeza kuwa askari hao waliokuwa kwenye magari mawili ya FFU, waliitwa na kuhojiwa ofisini kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Kilimanjaro (RCO), Ramadhan Ng’anzi.
  
Zaidi ya magari kumi aina ya Fuso yaliyosheheni sukari ya magendo yamekuwa yakivuka mpaka kwenda nchini Kenya kila siku kutoka katika mji mdogo wa Himo kupitia njia ya Kwa Hussein hadi yalipo machimbo ya mchanga aina ya pozolana mita chache kutoka kituo cha forodha cha Holili na kuingia nchini Kenya kirahisi.

No comments:

Post a Comment