Mwanaharakati mashuhuri wa kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja, amekamatwa nchini Zambia kwa kuonekana kwenye televisheni akitaka uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja kutofanywa kuwa hatia.
Paul Kasonkomona alishatakiwa kwa kosa la ''kuwachochea watu kushiriki vitendo visivyokubalika,'' alisema mkuu wa polisi Solomon Jere.
Paul alikamatwa alipokuwa anaondoka nje ya studio hizo za kampuni ya kibinafsi ya Muvi.
Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, ni haramu nchini Zambia.
Wadadisi wanasema kuwa watu wengi, wanaamini kuwa ni kinyume na imani zao
Duru katika stesheni hiyo, mjini Lusaka zilisema kuwa polisi walijaribu kukatiza mahojiano lakini wakuu wa stesheni hiyo walikataa.
Katika ombi lililotolewa kwa rais wa Zambia Michael Sata, kundi moja la wanaharakati nchini Afrika Kusini Ndifuna Ukwazi, lilitaka kuachiliwa mara moja kwa bwana Kasonkomona.
Kundi hilo pia lilisema linataka serikali ya Zambia kuanzisha mara moja mpango wa kutofanya vitendo hivyo kuwa kinyume na sheria ikiwa itakuwa kati ya watu wazima licha ya jinsia yao.
Vitendo kama ulawiti na uhusiano wa mapenzi kati ya wanawake, vina adhabu ya miaka 15 au kufungwa maisha jela.
Wiki jana kikundi cha wapenzi wa jinsia moja kilijaribu kujisajili kama wanandoa lakini wakakatazwa na serikali ikaamuru kukamatwa kwa yeyote atakayepatikana akihusika na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
Muungano wa ulaya mwezi jana ulitoa msaada wa kifedha kwa mashirika yaliyotaka kuhamasisha kuhusu haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Zambia.
Mnamo mwaka 2011, Marekani na Uingereza zilionya kuwa zitatumia msaada wa kigeni kama kikwazo cha kutoa ufadhili kwa nchi za kiafrika ili kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.
Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi chache barani Afrika zilizohalalisha mapenzi ya jinia moja.
No comments:
Post a Comment