Wednesday, May 1, 2013

"NITAGOMBEA URAIS MWAKA 2015 ENDAPO WANANCHI WENGI WATANIOMBA NIFANYE HIVYO"....BENARD MEMBE




WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, amesema atakuwa tayari kuwania urais mwaka 2015, iwapo wananchi wataona anafaa na kumtaka afanye hivyo. 

Alisema hayo juzi wakati akijibu maswali ya mwandishi wa habari hii mjini Iringa, baada ya kumalizika kwa kongamano la vyuo vya elimu ya juu mkoani hapa, lililofanyika katika ukumbi wa St. Dominic.

Membe aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, alisema ingawa muda wa kufanya uamuzi kuhusu mwaka 2015 bado na chama hakijatoa utaratibu, lakini atasubiri ushauri wa Watanzania.

"Naomba kurudia, mimi nilishapata kuueleza umma kuwa muda bado haujafika wa kutangaza kugombea urais ...ila nasema hivi natarajia sana ushauri wa Watanzania. 


“Iwapo Watanzania wataniona nafaa na kunitaka nigombee, nitapima mawazo yao na iwapo ni wananchi wengi watakaoniunga mkono kutaka nigombee, basi nitachukua fomu na kuijaza ili nigombee nafasi hiyo kwani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu," alisema Waziri Membe.

Maadili ya wabunge Membe alisema hali ya kisiasa nchini inakwenda vibaya kutokana na kila mtu kuzungumza mambo bila kujitathmini. 


Alisema mbaya zaidi hata baadhi ya wabunge wa CCM, nao wamekuwa si msaada kwa chama, kutokana na kuzungumza mambo dhidi ya Serikali na chama.

Membe alisema amepata kukaa bungeni kwa zaidi ya miaka 15 tangu Bunge la Spika Pius Msekwa, hadi sasa chini ya Spika Anne Makinda, ila anachokiona ni baadhi ya wabunge kukosa maadili na kuzungumza mambo bila kuzingatia kanuni za Bunge, jambo ambalo ni hatari zaidi.

Alisema Bunge linalotazamwa na Watanzania, ni lazima liwe la mfano wa kuigwa na lenye kuzingatia maadili katika kuzungumza, lakini sasa ndio maana Bunge linaendelea kupoteza mwelekeo. 


"Bunge linapoteza mwelekeo kutokana na mawazo ya baadhi ya wabunge wanaofikiri wakisema ovyo na kutumia lugha kali katika kuzungumza, wao ndio wanaonekana ni wabunge bora kitu ambacho hakipo.

“Mbunge ni pamoja na kujiheshimu na kutumia lugha nzuri katika kuwakilisha wapiga kura wako bungeni," alisema.


Membe alisema kutotumia busara katika kujadili mambo bungeni, si ubunge mzuri na bora watambue wazi kuwa wananchi wao wanawatazama na hukumu yao itatolewa mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu kama hicho wanachokifanya, ni kuwakilisha wananchi au kujiwakilisha.


"Nawaomba wabunge wawe wazalendo, wawakilishe wananchi waliowatuma badala ya kuligeuza Bunge kama sehemu ya kuonesha ujuzi wa kuzungumza ovyo.

“Nasema tuogope wananchi, mwaka 2015 watatoa adhabu kwa kila mbunge na kwa sasa wananchi wanasikiliza na kutazama ila muda ukifika watakuacha," alisema.

Alisema wabunge wengi ni vijana na wanafikiri kusema vibaya juu ya CCM ndio ubunge bora, ila watu watafanya uchunguzi wa kutembelea jimbo la mbunge husika na kuangalia amefanya nini katika jimbo lake na watampima kwa kazi aliyofanya na si ukali bungeni.


Alisifu baadhi ya wabunge wa CCM, kwamba wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika majimbo yao, kwa chama na Serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete, kwa kusukuma mbele maendeleo ya Taifa, ila baadhi yao wapo kwa ajili ya kuonesha uwezo wa kusema ovyo.

No comments:

Post a Comment