Sunday, April 28, 2013

BAJETI KIPORO WIZARA YA MAJI YATINGA TENA BUNGENI LEO





Mkutano wa 11 unaendeleo leo mjini Dodoma, ambapo Bajeti ya Wizara ya Maji iliyokwama kupitishwa baada ya wabunge kuigomea, inatarajiwa kuwasilishwa, ikiwa na  maboresho, hususani eneo la nyongeza ya fedha katika miradi ya maji.

Bajeti hiyo ilitarajiwa kupitishwa tangu Alhamisi wiki  iliyopita, lakini kutokana na ufinyu wa fedha zilizotengwa, takribani wabunge wote waliochangia mjadala wake, wakiwemo wa CCM, waligoma kuiunga mkono.
 
Kutokana na hali hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema suala la maji haliwezi kufanyiwa utani na kuitaka Wizara ya Maji, Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha, kufanyia kazi suala hilo na walete majibu ya uhakika.
 
Leo wabunge hao wanatarajia upande wa Serikali kuwasilisha bajeti hiyo, ikiwa na maboresho mapya ya nyongeza ya fedha za miradi inayotarajiwa kufikia zaidi ya Sh milioni 185, ambazo wabunge hao walipendekeza ili kutekeleza miradi ya maji na kupunguza tatizo la maji katika maeneo yao.
 
Wakati akiiwasilisha makadirio ya bajeti hiyo wiki iliyopita bungeni, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alibainisha kuwa Wizara hiyo imetengewa Sh bilioni 398, fedha ambazo wabunge hao walibainisha kuwa hazitoshi, ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya maji nchini.
 
Wakati akiahirisha mjadala huo wa Bajeti ya Maji, Spika alisema: “Naona sasa mahitaji ya wabunge wote na wananchi kwa ujumla ni bajeti hii, kwa kweli iboreshwe ili kufikia malengo stahiki katika maeneo yetu.”

Viongozi wa Wizara ya Fedha, Kamati ya Bajeti na Wizara ya Maji, kwa takribani siku tatu, walikutana na kujadili suala hilo na namna ya kupata fedha za kuongezea kwenye bajeti hiyo, huku wabunge wa CCM nao wakikutana ili kuwekana sawa, kutokana na kilichotokea bungeni kuhusu bajeti hiyo.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alipongeza hatua za wabunge hasa wa CCM, kuweka itikadi zao pembeni na kuungana pamoja kuikataa bajeti hiyo, ambayo haikuwa na mfumo mzuri wa kumaliza tatizo la maji nchini.
Hata hivyo, alipendekeza leo Serikali ije na maboresho yatakayoainisha namna ya kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo, uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, ambao katika eneo la maji utahitaji Sh bilioni 500.

Pamoja na mjadala wa Bajeti ya Maji kuendelea leo, pia Wizara ya Maliasili na Utalii, inatarajiwa kuwasilisha bajeti yake ya mwaka 2013/2014, itakayojadiliwa kwa siku mbili, ambapo wabunge wengi wanatarajia kuzungumzia suala la mgogoro wa ardhi Loliondo.

Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria nayo inatarajiwa kuwasilishwa kesho huku suala la Mabaraza ya Katiba likiwa ajenda kuu, iliyopaniwa kujadiliwa hasa na wapinzani, ambao wamekuwa wakilalamikia mchakato wake wa uchaguzi, kwamba umekuwa ukitawaliwa zaidi na masuala ya siasa.

Katika wiki hii, bajeti nyingine itakayojadiliwa ni ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambayo itajadiliwa kwa siku moja.

No comments:

Post a Comment