Friday, April 19, 2013

WASSIRA AMTETEA RAIS KIKWETE KUWA YEYE SI MUASISI WA UDINI HAPA NCHINI



WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, amepinga vikali madai yaliyotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema) akidai kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye muasisi wa udini. 

Akizungumza bungeni jana, Wassira alimshangaa Lema kwa kutoa kauli hiyo, ambayo alisema imemvunjia heshima rais na kwamba hiyo ni kinyume cha Katiba. 

“Mimi nimesikitishwa sana na kauli ya Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) aliyoitoa jana (juzi) humu ndani akisema Rais Kikwete ndiye mwasisi wa suala la udini.

“Nimeshangazwa kwa sababu tuhuma hizi dhidi ya mkuu wa nchi ni nzito hazipaswi kusemwa tu hivi hivi, mimi nafikiri hili Bunge sasa sijui tunakwenda wapi.

“Kwa maneno haya Lema amevunja Katiba kwa kusema makali kiasi hiki dhidi ya rais, tunataka Lema alete ushahidi juu ya tuhuma hizi.

“Rais anapoteua wakuu wa mikoa na wilaya anashauriana na waziri mkuu ambaye huyu tuliyenaye leo ni mkiristo.

“Anapoteua makatibu wakuu anashauriana na katibu mkuu kiongozi, Ofisi ya Rais ukimwondoa yeye mwenyewe waliobaki wote ni Wakristo. Huo udini uko wapi?

“Lema lazima ajue kuna hotuba za kijiweni na hotuba za bungeni lazima atofautishwe, lakini hapa kinachofanyika watu wanaleta hotuba za kijiweni badala ya hotuba za Bunge.

“Mgogoro wa kuchinja, mimi nilikwenda kule Geita kwenye mgogoro tukamaliza huu mgogoro kwa kuwashirikisha waumini wa dini, nashanga Lema anasema Serikali haijachukua hatua yoyote.

“Namtaka Lema popote alipo ajue kwamba Serikali inafanya kazi kwa utaratibu, alitaka tuende pale tutoe amri, asubiri atakapoingia madarakani sijui ni lini ndipo aendeshe Serikali kwa amri tu bila kushirikisha watu

Wassira alikuwa akihitimisha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi) ambapo alisema hisia za udini nchini zimechochewa zaidi kupitia mikanda (CD) mbalimbali ya kidini.

Alisema Kanda hizo zilikuwa zikihamasisha na kuwataja viongozi na maaskofu wa Kikristo, lakini zote zimekamatwa na serikali imeahidi kuwalinda viongozi hao.

Alisema kanda zote zimekamatwa na yeyote mwenye nazo akikamatwa atachukuliwa kuwa ni mchochezi sawa na waliotengeneza kanda hizo.

“Wale waliokimbilia nje ya nchi tunaendelea kuwatafuta kwa kutumia polisi wa kimataifa (Interpol) ili waje kujibu kesi ya uchochezi.

“Mheshimiwa Spika, hata hivyo udini unaoenezwa bado haujavuruga maisha ya wananchi, kwamba wananchi huko mitaani wanaendelea kushirikiana vizuri, hakuna kubaguana. Na nadhani tatizo halijawa kubwa kupindukia.

“Suala la udini linakuzwa zaidi na watu wenye malengo mabaya ya kisiasa, tangu huko nyumba hata Zanzibar yenye asilimia zaidi ya 90 waislamu haijawahi kuitangaza Zanzibar kuwa ni nchi ya kiislamu.

“Udini ulichochewa na wanasiasa mwaka 2010 kwa sababu ya watu kutaka madaraka. Mwaka huo haukuwa mzuri sana, lakini tuyaache, yaliyopita si ndwele.
 

“Wahenga walisema, usipoziba ufa utajenga ukuta, baba wa taifa, hayati Mwalimu Nyerere alisema ukisikia wanaopaza zaidi sauti za udini ndiyo wanaoueneza, kwa hiyo tuwe makini na wanaopiga kelele juu ya jambo hilo.

“Katika suala hili, ni vema Bunge litafute namna bora ya kushughulikia suala hili ili lisiendelee kuwa kikwazo kwa amani ya nchi yetu” alisema Wassira

No comments:

Post a Comment